Heart Team Africa Foundation

Heart Team Africa Foundation

In the joy of others lies our own

19 Oct

VODACOM Yaingia Mkataba na HTAF kwa Ajili ya Kurejesha Tabasamu kwa Watoto Wenye Magonjwa ya Moyo

Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesaini mkataba wa ushirikiano na taasisi ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kwa lengo la kusaidia matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo, ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha afya ya watoto na kurejesha tabasamu katika familia nyingi. Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mkurugenzi Mtendaji wa HTAF, Naizihijwa Majani, ameishukuru Vodacom kwa moyo wa ushirikiano na mchango wao katika kusaidia watoto wenye uhitaji mkubwa wa huduma za kibingwa za afya ya moyo. "Tunatoa shukrani za dhati kwa Vodacom kwa kuamua kushirikiana nasi katika dhamira hii ya kuokoa maisha ya watoto. Kwa kupitia ushirikiano huu, Vodacom itagharamia asilimia 30 ya gharama za matibabu kwa kila mtoto anayepatiwa huduma kupitia mpango huu," alisema Majani. Mkataba huu unalenga kutoa msaada wa kiafya kwa watoto ambao wengi wao hutoka katika familia zisizo na uwezo wa kugharamia matibabu ya moyo, ambayo mara nyingi huhitaji rufaa na uangalizi maalum kutoka kwa madaktari bingwa. Kupitia usaidizi huu, watoto wengi wataweza kupatiwa matibabu kwa wakati na kurejea kwenye maisha ya kawaida ya ujana, shule na ndoto zao. Ushirikiano kati ya HTAF na Vodacom ni sehemu ya juhudi za pamoja za sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali katika kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa wote, hasa kwa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi. Mpango huu unaendana na malengo ya maendeleo endelevu (SDGs), hususan lengo namba 3 la kuhakikisha afya bora na ustawi kwa wote, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwekeza katika afya ya watoto kama msingi wa taifa lenye nguvu na lenye matumaini ya baadaye.

recent news